Pages

Wednesday, July 31, 2013

Unaweza kuepuka magonjwa ya Saratani kwa njia hii

LISHE SAHIHI INAVYOWEZA KUKUEPUSHA NA SARATANI



Wataalamu wa masuala ya afya wanaamini kuwa robo ya vifo vyote vinavyotokana na saratani husababishwa na ulaji vyakula usiosahihi na unene wa kupita kiasi (obesity).

Aidha, inaaminika kuwa milo yetu ya kila siku inachangia kwa kiasi kikubwa saratani za aina mbalimbali zikiwemo za tumbo, mdomo na matiti.

Hata hivyo, unaweza kupunguza hatari ya kupatwa na saratani kwa kuzingatia ulaji sashihi kama ambavyo tumekuwa tukieleza kila wiki katika makala yetu na kama itakavyosisitizwa tena leo katika makala haya.

Wataalamu wetu wanashauri watu wapende kula vyakula vyenye ‘faiba’ nyingi (ufumwele), kama matunda, mboga za majani na kula kwa uchache sana nyama nyekundu na vyakula vya kusindikwa. Vyakula vya kwenye makopo vinapigwa vita kutokana na kemikali zinazotumika kuhifadhia vyakula hivyo.

Katika makala ya leo tutajaribu kueleza ni kwa kiasi gani vyakula unavyokula vinaweza kukuongozea hatari ya kupata saratani. Aidha tutaelezea ni ulaji upi sahihi unaoweza kukuepusha na saratani.

UHUSIANO KATI YA LISHE NA SARATANI.
Uhusiano kati ya saratani na lishe ni suala tete na gumu kulibainisha. Hali hii inatokana na ukweli kwamba milo yetu ina mchanganyiko wa vyakula vingi na virutubisho mchanganyiko. Vyakula vingi huchangia hatari ya mtu kupata saratani, hasa vinapochanganywa na vingine, ingawa wakati mwingine mtu huweza kupata saratani kwa kurithi vinasaba ‘genes’.

Wanasayansi wengi wanafanya kazi usiku na mchana ili kujua ni vyakula gani hasa vinaweza kutulinda dhidi ya saratani na vyakula vipi vinaweza kutusababishia satarani, baadhi ya tafiti zimeshaweza kulijua hilo na tafiti zaidi bado zinaendelea kufanywa.

Kwa sasa, vipo vyakula vinavyofahamika kwa ubora ambavyo kila mtu anapaswa kuvila. Tunaelewa pia kuwa mlo sahihi unasaidia kudhibiti uzito wa mwili ambao ukidhibitiwa vizuri, unamuondolea mtu hatari ya kupata saratani za aina mbalimbali.

MATUNDA NA MBOGA MBOGA
Ulaji wa matunda na mboga kwa wingi kunapunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa saratani, hasa saratani ya viungo vya kwenye mfumo wa kupitishia chakula, kama vile mdomo, tumbo na njia ya haja kubwa. Hata hivyo matunda na mboga vinaweza visiondoe kabisa hatari ya mtu kupata saratani zinazosababishwa na ‘homoni’ kama saratani ya ziwa na kizazi.
USHAURI SAHIHI: Penda kula angalau milo mitano ya matunda kwa siku na mboga tofauti tofauti. Ulaji wa matunda ya rangi tofauti husaidia kupata aina mbalimbali za vitamini na madini ambayo yataupa kinga mwili wako dhidi ya maradhi mbalimbali.

NYAMA
Ulaji kidogo wa nyama nyekundu na za kusindika husaidia kupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo, kwani vyakula hivyo si vya kupenda kula kwa wingi, japo ni vitamu mdomoni.

Kuwa na tabia ya kupenda sana kula nyama nyekundu na za kusindika kunaongeza hatari ya mtu kupata saratani ya tumbo. Nyama nyekundu zinajumuisha pia nyama ya nguruwe, iwe ya vipande au kusagwa pamoja na ‘soseji’. Nyama nyeupe, kama vile ya kuku na samaki hazina hatari.

USHAURI: Kula kiasi kidogo sana cha nyama nyekundu na za kusindika. Badilisha kwa kula maharage au kunde badala ya nyama. Unapopika nyama, tumia joto kiasi au mvuke, upikaji nyama kwa moto mkali mpaka inaungua kunaweza kuzalisha kemikali za saratani.

SAMAKI
Ulaji kwa wingi wa samaki kunaweza kukupunguzia hatari ya kupata saratani. Pendelea kula samaki zaidi kuliko nyama nyekundu au za kusindika kama tulivyozianisha hapo juu. Samaki wa kuoka, kuchemsha ni bora zaidi.

VYAKULA VYENYE CHUMVI
Vyakula vyenye chumvi nyingi au vyakula vilivyohifadhiwa kwa chumvi, vinaongeza hatari ya mtu kupata satarani ya utumbo na koo. Hata hivyo, tafiti zingine zinaonesha kuwa chumvi ya mezani inayotumika kupikia au kuongezea ladha haina uwezekano wa kuchangia saratani, lakini chumvi nyingi huongeza shinikizo la damu na hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na hatimaye kiharusi.

USHAURI: Usipende kula vyakula vyenye chumvi nyingi au vile vilivyohifadhiwa kwa kutumia chumvi. Unaponunua vyakula vya kusindika, kagua kiasi cha chumvi kulichomo. Chumvi inaweza kufichwa mahali ambako hukutegemea, hasa kwa vyakula vinavyochanganywa na sukari.

VYAKULA BORA
Vyakula bora vyenye kiwango kikubwa cha ‘faiba’ (ufumwele) hupunguza hatari ya mtu kupatwa na satarani. Vyakula hivyo ni pamoja na matunda, mboga mboga, nafaka zisizokobolewa na mikate inayotengenezwa kutokana na ngano isiyokobolewa (whole bread), mchele mweusi, kunde, n.k.

MAFUTA
Mafuta ni muhimu kwa mwili wa binadamu, lakini haishauriwi mtu kupenda kula vyakula vyenye mafuta mengi, hasa mafuta ya wanyama ambayo siyo mazuri kiafya. Kwa ujumla kanuni ya ulaji sahihi ni kula matunda na mboga kwa wingi, vyakula vitokanavyo na nafaka zisizokobolewa na jamii yote ya kunde na maharage, vyakula hivyo vimethibitisha kupunguza kwa kiwango kikubwa hatari ya mtu kupata saratani

No comments:

Post a Comment