Ijue siri ya kuwa na kinga ya mwili imara
Kinga ya mwili ndiyo kila kitu katika afya ya binadamu. Kinga ya mwili ni ile hali ya mwili kuwa na uwezo wa kujikinga wenyewe dhidi ya maradhi mbalimbali. Ukiwa na kinga imara ya mwili, huwezi kuugua mara kwa mara.
Kuumwa mara kwa mara ni dalili tosha kuwa kinga yako ya mwili imeshuka na hivyo unahitaji kuchukua hatua za kuiimarisha. Mungu aliuumba mwili ukiwa na uwezo wake wa kujikinga na magonjwa yote, ikiwa tu utaupatia vyakula inavyohitaji kuimarisha kinga yake.
Hapo ndipo unapokuja umuhimu wa kujua ni vyakula gani vina imarisha kinga na vyakula gani vinapunguza nguvu ya kinga ya mwili. Leo tunazungumza kuhusu kinga ya mwili kwa kuangalia aina ya vyakula vya kuepuka au kuzingatia ili kuupa mwili uwezo wa kujikinga na maradhi. Na kumbuka kinga ni bora na rahisi kuliko tiba!
EPUKA ULAJI WA SUKARI
Kama kuna kitu kinapendawa sana na watu wengi ni sukari, lakini siyo nzuri kwa afya yetu inapotumiwa kupita kiwango. Kiwango cha kawaida cha sukari kinachoruhusiwa kutumiwa ni kijiko kimoja kidogo (teaspoon), kinapozidi hapo huwa kinachangia kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili. Inaelezwa kuwa chupa moja ya soda ina karibu vijiko 6 vya sukari. Hivyo kama wewe ni mnywaji mkubwa wa soda na vinywaji vingine vya aina hiyo, utaona ni kiasi gani unaharibu kinga yako ya mwili kadri unavyotumia kila siku!
EPUPA UNYWAJI WA KAHAWA
Kirutubisho kiitwacho ‘caffeine’ kilichomo kwenye kahawa kinaweza kuondoa virutubisho muhimu katika mwili kama vile calcium, magnesium na potassium. Kahawa huweza pia kuathiri mfumo wetu wa fahamu na kusababisha wasiwasi na ukosefu wa usingizi.
Hivyo unywaji wa mara kwa mara na wa kiasi kingi wa kahawa huukosesha mwili kupumzika, ili hali kupumzika pamoja na kulala usingizi ni vitu muhimu sana katika uponyaji wa maradhi mengi ya mwili kwa njia ya asili. (Natural healing).
USINYWE KILEVI
Unywaji wa pombe kupita kiasi ni sumu kwa miili yetu. Kitu cha kwanza kuathirika na ulevi wa kupita kiasi ni ini, halikadhalika mfumo wa fahamu nao huathirika, hali hiyo hudumaza pia uzalishaji wa seli za damu mwilini (blood cells).
JIHADHARI NA VYAKULA VIBICHI
Osha vizuri na kwa umakini sana matunda kabla ya kuyala. Kuna bakteria wa kila aina kwenye vyakula vibichi, yakiwemo matunda, hivyo kuosha matunda kwa makini ni muhimu. Pia ulaji wa mayai mabichi au yaliyopikwa na kuiva kiasi huweza kuwa na bakteria, hivyo kinga ya mwili kudhoofika na wale wenye kinga dhaifu wanaweza kupatwa na magonjwa ya mlipuko.
EPUKA, CHIPS, VYAKULA VYA KUKAANGA NA KUOKA
Vyakula vya kukaanga kama vile chips na vinginevyo, pamoja na vyakula vya kuoka huwa na mafuta mabaya ambayo huwa na tabia ya kutengeneza magonjwa mwilini (fee radicals) ambayo huathiri mfumo wa kinga ya mwili pamoja na chembechembe za nasaba (DNA). Vyakula hivi ni vya kuliwa kwa nadra sana au kuepukwa kabisa.
EPUKA VYAKULA VYA MAKOPO
Epuka ulaji wa vyakula vya kwenye makopo na badala yake pendelea kula vyakula ‘fresh’ na vya asili. Ulaji wa vyakula vya asili, hasa vyakula vitokanavyo na nafaka zisizokobolewa, huwa na idadi kubwa ya vitamini, madini na kamba-lishe ambazo ni muhimu sana katika kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili.
KULA KWA WINGI MBOGA- MBOGA
Kula kwa wingi mboga za majani na matunda. Zabibu ni miongoni mwa matunda yanayotajwa kuwa na virutubisho vingi vyenye uwezo wa kuzuia mlaji asipatwe na ugonjwa wa saratani. Aidha, inashauriwa kutokula kwa wingi matunda yenye kiwango kikubwa cha sukari, kama vile ndizi na maembe. Ulaji wa matunda haya uwe ni kwa uchache.
TUMIA VIUNGO HIVI KILA SIKU
Vitunguu maji, vitunguu saumu, tangawizi, uyoga, n.k, ni viungo muhimu vya mboga ambavyo vinasaidia sana kuimarisha kinga ya mwili, hivyo inashauriwa kuvitumia kila siku katika milo yetu.
KUNYWA MAJI ‘VUGUVUGU’ MENGI KILA SIKU
Unapokunywa maji usinywe maji yaliyoganda au ya baridi sana. Unapokunywa maji baridi unaupa kazi mwili wako wa kuyachemsha tena hadi kufikia nyuzi joto 98.6, hivyo pendelea kunywa maji ya uvuguvugu kiasi cha lita moja hadi tatu kwa siku.
Mwili unapokuwa na maji ya kutosha, hurahisisha kazi ya ini na figo ya kuondoa sumu mwilini na kuimarisha kiwango cha sukari mwilini. Pia maji hufanya utumbo mpana wakati wote kuwa na unyevu ambao husaidia kupambana na virusi vya aina mbalimbali.
PATA MUDA WA KULALA
Kutegemeana na umri wa mtu, binadamu anatakiwa kupata usingizi kwa muda wa saa 6 hadi 10 kwa siku. Usingizi hujenga uwiano mzuri wa homoni mwilini na hujenga uzito sahihi wa mwili na kujenga ngozi nyororo. Yakizingatiwa kwa vitendo mambo yaliyotajwa katika makala haya, kinga yako itaimarika na kamwe hutasumbuliwa mara kwa mara na magonjwa ya kawaida.
No comments:
Post a Comment