Eti Liverpool imekaribia kuuzwa?
Siku chache baada ya kukaribia kumuuza nyota wake Luis Suarez,
wamiliki wa klabu ya Liverpool ambao ni kampuni ya Fenway Sports Group
wako mbioni kuiuza klabu hiyo.
Kampuni hiyo yenye maskani yake Boston Marekani ambayo inaongozwa na
mfanyabiashara John W. Henry, iliinunua klabu ya Liverpool toka kwa
wafanyabiashara George Gillett na Tom Hicks huku wakiwa na mtazamo wa
kibiashara wa kutengeneza fedha kupitia klabu hiyo jambo ambalo
halijatokea katika kipindi cha miaka minne ya umiliki wao.
John W. Henry aliinunua Liverpool kwa paundi milioni 300 na anataka
kuiuza kwa paundi milioni 350 ambapo kwa mujibu wa taarifa toka benki
moja Marekani, klabu hiyo imewekwa sokoni kwa mtu yoyote atakaekuwa
tayari kuinunua.
Henry anaonekana kuchoshwa na kitendo cha kutotimia kwa malengo ya
kibiashara aliyokuwa ameiwekea Liverpool ambapo katika kipindi cha miaka
minne klabu hiyo bado imeshindwa kushiriki ligi ya mabingwa na
haijaweza kuwa na ubora wa ubingwa wa ligi ya England.
Pamoja na hayo Liverpool pia imekuwa ikipata hasara kwenye soko la
wachezaji ambapo mara kadhaa imekuwa ikishindwa kurudisha thamani ya
fedha zinazotumika kwenye matokeo uwanjani na hata kwenye mauzo ya
wachezaji ambapo moja ya hasara kubwa ambazo zimemkera mmiliki John W
Henry ni kitendo cha kununuliwa kwa Andy Caroll kwa paundi milioni 35
kabla ya kumuuza kwa paundi milioni 19 huku akiwa hajawahi kufanya
vizuri kulingana na thamani ya fedha iliyotumika kumsajili.
Uongozi wa Fenway Sports Group ulikutana na kampuni ya mafuta ya
Saudi Aramco ya huko Saudi Arabia kujadiliana uwezekano wa kampuni hiyo
ya mafuta kuidhamini Liverpool lakini vingozi wa Saudi walikuja na wazo
la kuinunua kabisa klabu hiyo ambapo hadi sasa kampuni mbili
zinazomilikiwa na mabilionea wa kimarekani zimeripotiwa kuwa na wazo la
kununua Liverpool lakini hakujakuwa na ofa rasmi.
No comments:
Post a Comment