ALIYOYASEMA EDWARD MORINGE SOKOINE
Ndugu Edward Moringe Sokoine (01/08/1938-12/04/1984) alikuwa Waziri
Mkuu wa aina yake nchini Tanzania. Aliongoza katika kipindi ambacho nchi
ilikuwa katika hali ngumu sana ya kiuchumi. Leo ni miaka 27 toka Taifa
limpoteze shujaa huyu. Katika kuenzi fikra zake ambazo bado zinahitajika
sana leo, Udadisi inakuletea nukuu zifuatazo kama ilivyozipata kutoka
kwenye Kitabu cha Edward Moringe Sokoine: Kiongozi wa Watu Aliyejitolea kilichoandikwa na Luteni Kanali Albert N. Kigadye mnamo mwaka 1984:
"Ole
wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa
siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na
Wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao.
Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda
kama vitendo vyao viovu" - Edward Moringe Sokoine, 26 Machi 1983
"Juu
ya suala hili la mapato kutolingana na matumizi ni kwamba tungependa
kupunguza uongezaji wa wataalam wasiohitajika katika Serikali na katika
mashirika ya umma mpaka hapo hali yetu ya uchumi itakapokuwa katika hali
nzuri" - Edward Moringe Sokoine, 23 Oktoba 1982
"Serikali
inasimamia bei, lakini Serikali yetu itakwenda mpaka itasimamia bei ya
mhogo, dagaa na bei ya kila kitu? Haiwezekani, vitu vingine ni lazima
vizalishwe kwa wingi ili bei yenyewe iweze kujirekebisha" - Edward
Moringe Sokoine, 24 Septemba 1983
"Wajibu
wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni kujilisha mwenyewe.
Si wajibu wa Taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na
janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze
kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa" - Edward Moringe
Sokoine, 4 Oktoba 1983
"Vijana leo wengi
wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi miaka thelathini hadi
arobaini. Lakini wanaitaka Serikali ndiyo iwaulize mali hiyo wameipata
wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanae, 'mali hii umeipata wapi?'" -
Edward Moringe Sokoine, 23 Oktoba 1983
"Katika
nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha
kulinda haki na maslahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni
chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio
wengi" - Edward Moringe Sokoine, 1 Februari 1977
No comments:
Post a Comment