I Have A Dream: Martin Luther King Jr Day na Harakati Tanzania ya Sasa
Kilichonisukuma kuandika post hii ni
habari niliyoiona kwenye runinga katika kipindi cha Anderson Cooper 360
(katika kituo cha CNN) kwamba mwanabodi wa taasisi moja ya elimu huko
Marekani amekuwa akimshambulia mwanaharakati Dkt Martin Luther Jr,ambaye
jana ilikuwa siku ya kumbukumbu yake (Martin Luther King Jr Day).
Mashambulizi hayo dhidi ya Dkt King
yalijumuisha madai kama "mwanaharakati huyo hakuwa Dokta"-ikimaanisha si
sahihi kuweka kitangulizi hicho kabla ya jina lake,na "alikuwa
mkomunisti"- na kwa wahafidhina nchini Marekani,ukomunisti unachukuliwa
kama Unazi.
Tukio hilo ni mwendelezo tu wa
mashambulizi dhidi ya Dkt King hususan kutoka kwa wanaokumbatia hisia za
ubaguzi wa rangi. Lakini kama kuna mtu aliyekuwa "obsessed" zaidi na
jitihada za kumuumbua Dkt King basi si mwingine bali Mkrugunzi wa zamani
wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) J.Edgar Hoover. Inaelezwa kuwa
shushushu huyo alijitahidi kadri alivyoweza kufanikisha azma yake hiyo
muflis, ikiwa ni pamoja na kurekodi (bugging) maongezi ya Dk King
anayetambulika kama chachu ya mapambano (ya amani) na mafanikio ya
Wamarekani Weusi kukubalika katika nchi hiyo (kwa kiasi kikubwa).Hata
mafanikio ya Barack Obama,Mweusi wa kwanza kushika nafasi ya urais wa
Marekani yanahusishwa kwa kiasi kikubwa na harakati na changamoto
zilizoanzishwa na Dkt King.
Tanzania yetu ya leo inaweza kabisa
kulinganishwa na hali ilivyokuwa katika Marekani ya enzi za akina Dkt
King ambapo ubaguzi wa rangi ulikuwa umeshamiri vilivyo.Huko nyumbani,na
hasa baada ya kifo cha Baba wa Taifa-aliyekuwa muumini mkubwa wa usawa
wa binadamu-wengi wa wanasiasa wetu wamekuwa bize kutengeneza mgawanyiko
katika jamii kati ya wenye nacho na wasio nacho, vigogo na walalahoi, na
katika zama hizi za Kikwete, tumeshuhudia mgawanyiko mkubwa zaidi katika
jamii; mafisadi dhidi ya wananchi wa kawaida, na hivi karibuni
CCM, Serikali yake na vyombo vyake vya dola dhidi ya wananchi na
wapinzani (hususan Chadema) na haki zao.
Lakini pengine la kutisha zaidi ni
vuguvugu linalochochewa na CCM ya Kikwete na mafisadi anaowalea la
kuwagawanya Watanzania kwa misingi ya imani zao za kidini. Kila mwenye
macho na masikio ameona na kusikia kauli mbalimbali za msigishano kati
ya viongozi wa CCM na baadhi ya viongozi wa Kanisa kwa upande mmoja,na
kwa upande mwingine ni msuguano (unaoelekea kukua) wa kimtizamo kati ya
baadhi ya viongozi wa Kanisa na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam.
Kama ambavyo nimerejea kwenye posts na
makala zangu kadhaa huko nyuma,suala hili tofauti za kidini kutumika
kwa maslahi ya kisiasa linanigusa sana,kitaaluma kama mwanafunzi wa
utafiti katika mahusiano ya siasa na dini,na kama raia wa Tanzania-nchi
ambayo licha ya kuwa na viungo (recipes) vinavyoweza kupelekea mgogoro
wa kijami kwa misingi ya kidini,angalau hali kwa ujumla imekuwa salama
(kwa maana ya kutokuwepo vurugu za aina hiyo).
Inapofikia mahala vyombo vya habari
vya umma vinatumika kusambaza ujumbe
wa kuchochea mvurugano katika jamii badala ya kuhamasisha maelewano,ni
dhahiri kuwa tunakoelekea si kwema.Vyombo hivi vya habari
vinavyoendeshwa kwa fedha za walipakodi pasipo kujali itikadi zao za
kisiasa vinaanza kuchukua mwelekeo wa gazeti la Kangura na vituo vya radio vya Radio Rwanda na Radio Télévision Libre des Mille Collines (RTLM)
ambavyo vilichangia sana kuhamaisha propaganda za chuki dhidi ya
Watutsi zilizopelekea mauaji ya kimbari nchini Rwanda kati ya mwaka
1994-95.
Nirejee kwa Dkt King na funzo
linaloweza kusaidia katika harakati za mapambano dhidi ya udhalimu wa
Kikwete na CCM yake inayoendeshwa kishkaji. Pamoja na jitihada na nguvu
kubwa iliyotumika kumdhibiti,na hatimaye kuuawa,mbegu alizopanda
mwanaharakati huyo zimefanikiwa kuzalisha watu kama
Obama, Oprah, Condoleeza Rice, Collin Powell n.k ambao kwa hakika
wasingeweza kujichomoza katika mfumo wa kibaguzi uliowabagua Weusi
katika kila nyanja ya maisha nchini Marekani. Kama ambavyo Dk King aliandamwa na FBI
na J. Edgar Hoover ndivyo wazalendo kama Dkt Wilbroad Slaa walivyojikuta
wakiandamwa na taasisi za serikali katika kila wanalofanya,huku baadhi
ya waendaji wa taasisi hizo wakidiriki hata kuvunja "miiko"
waliyojiwekea ili waweze kumshamshambulia Dkt Slaa (rejea kauli ya Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka).Na
kama ambavyo wabaguzi wa rangi wanavyoendelea kubomoa misingi
iliyowekwa na Dkt King, ndivyo Kikwete akisaidiwa na mafisadi
anaowalea-plus vyombo vyao vya habari-wanavyofanya kila wawezalo
kudhoofisha harakati za kuwakomboa Watanzania kutoka katika himaya ya
ufisadi,ukiukwaji haki za binadamu na umasikini wa kupindukia.
Usihadaike na kauli za watu
wanajifanya kutahadharisha kuwa mjadala wa Katiba mpya usiwe chanzo cha
kuhaarisha amani kwani yayumkinika kuamini kuwa wale wote wanaohusishwa
na ufisadi wasingependelea kuona tunakuwa na Katiba mpya inayompa
mamlaka mwananchi wa kawaida kuwa mwenye nchi halisi badala ya hali
ilivyo sasa ambapo nchi yetu imekuwa kama kampuni binafsi ya
mafisadi, wakiipelekesha watakavyo na sheria zikibaki sheria tu isipokuwa
katika kukandamiza maandamano ya amani na kuminya haki za binadamu.
Licha ya kuuawa kwake,wengi wa
Wamarekani Weusi sasa wanafaidi matunda ya harakati za Dkt Martin Luther
King Jr. Vikwazo na upinzani wa kila hali dhidi ya harakati hizo
hakukumvunja moyo Dkt King na hata kifo chake hakiwazuia washirika na
watangulizi wake kuendeleza harakati hizo za kudai usawa wa
binadamu.Damu ya mashujaa iliyomwagika huko Arusha kutokana na unyama
waliofanyiwa na polisi wa Kikwete na IGP Mwema isipotee bure bali iwe
chemuchemu ya kudumu kuhakikisha kuwa hatimaye udhalimu na ufisadi wa
CCM na serikali yake unakomeshwa completely.
Kama Dkt Martin Luther King Jr aliweza, na Nelson Mandela akaweza pia-bila kusahau kuwa nasi pia tuliweza kumwondoa mkoloni na kumfurumusha nduli Idi Amin-basi kwa hakika harakati hizi za sasa zinaweza pia kufanikisha ndoto na malengo yetu ya kuwa na Tanzania tunayostahili kuwa nayo, na sio hii ya sasa inayoendeshwa kwa remote control na mafisadi huku wakiwatuza majambazi wa Dowans kwa mabilioni na "kuwazawadia" waandamaji wa amani risasi za kuwaua na kuwajeruhi
No comments:
Post a Comment