MMOJA AFARIKI KATIKA MAANDAMANO BRAZIL.
Raisi wa Brazil, Dilma
Rousseff ameitisha mkutano wa dharura leo ikiwa ni siku moja baada ya
muandamanaji kuuwawa na wengine zaidi ya milioni 1.25 wakiendelea
kuandamana nchi nzima wakidai huduma nzuri kwa jamii. Pilikapilika
hizo za uandamanaji ambazo mara nyingine zinaleta vurugu kubwa,
zinafanyika wakati nchi hiyo iikiwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la
Shirikisho inayoendelea ambayo huchezwa mwaka mmoja kabla ya Kombe la
Dunia. Raia wengi
wa Brazil wamekuwa wakigadhabika juu ya gharama kubwa za maandalizi
zilizotumika kwa ajili ya kuandaa na Kombe la Dunia 2014 na michuano ya
olimpiki kipindi cha kiangazi itakayofanyika jijini Rio de Janeiro 2016.
Jijini Rio
polisi wamekuwa wakipambana na waandamanaji hao ambao hujikusanya karibu
na Uwanja wa Maracana ambapo wamekuwa wakilazimika kutumia mabomu ya
machozi na risasi za moto ili kuwatawanya.
PIRLO KUIKOSA BRAZIL.
Kiungo mahiri wa
kimataifa wa Italia, Andrea Pirlo anatarajiwa kukosa mchezo wa mwisho wa
kundi A dhidi ya wenyeji Brazil kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho
baada ya kupata majeraha ya msuli katika mguu wake wa kulia. Kocha
wa viungo wa nchi hiyo, Enrico Castellacci amesema anamatumaini Pirlo
anaweza kurejea katika mechi ya nusu fainali lakini ukijumuisha na
kukosekana kwa Daniele De Rossi ambaye naye pia atakosa mchezo wa
mwishoni itabidi kocha wa timu hiyo Cesar Prandelli abadili kikosi
chake. Italia
ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibugiza Japan ka mabao 4-3 na
kufikisha alama sawa na Brazil katika kundi lao ambapo mechi ya mwisho
ndio itakayoamua nani atasonga mbele kama mshindi wa kundi. Timu
zote mbili itabidi zipange vikosi vyao kamili ili kutafuta ushindi na
kuepuka kukutana na bingwa wa dunia Hispania katika hatua ya nusu
fainali.
HISPANIA WAPORWA HOTELINI WAKATI WAKIWA KWENYE MECHI.
Vyombo vya habari nchini
Hispania vimeripoti kuwa wachezaji sita wa timu ya taifa ya Hispania
wameibiwa fedha zao katika vyumba walivyofikia katika hoteli moja jijini
Recife wakati wanacheza mchezo wao ufunguzi wa Kombe la Shirikisho
dhidi ya Uruguay. Mojawapo
ya wachezaji waliokumbwa na mkasa huo ni beki wa Barcelona, Gerard
Pique ambaye aligundua kaibiwa wakati aliporejea chumbani kwake baada ya
mchezo dhidi ya Uruguay ambao walishinda kwa mabao 2-1. Msemaji
wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA, Pekka Odriozola alikiri kupata
taarifa hizo lakini wameziachia mamlaka husika kushughulikia na kisha
kuwaletea taarifa kamili. Hispania
ambao wako kundi B jana wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya
michuano hiyo kwa kishindi baada ya kuishindilia Tahiti kwa mabao 10-0
wakati wawakilishi pekee wa Afrika kwenye mashindano hayo walishindwa
kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha
mabao 2-1 kutoka kwa Uruguay.
MERCEDES WAFUNGIWA KUFANYA MAJARIBO MSIMU HUU.
Timu ya Marcedes
imefungiwa kufanya majaribio kwa madereva wake chipukizi kwa mwaka huu
pamoja na kupewa onyo kali kwa kosa la kufanyia majaribio magurudumu ya
Pirelli kinyume cha utaratibu. Kampuni
hiyo ya magurudumu ya Pirelli nayo pia imepewa onyo kwa kutumia gari
jipya linalotumiwa katika mashindano ya langalanga na dereva Lewis
Hamilton katika majaribio ya siku tatu waliyofanya nchini Hispania mwezi
uliopita. Kamati
maalumu ya uchunguzi wa suala hilo iliyoundwa na Chama cha Kimataifa
cha Langalanga-FIA kilichukua hatua hiyo baada ya kuwakuta Mercedes na
hatia ya kutenda kosa hilo ambalo ni kinyume cha utaratibu wa mashindano
hayo. Katika
sheria za langalanga timu yoyote hairuhusiwi kufanya majaribio
magurudumu kwa zaidi ya kilometa 1000 pindi msimu wa mshindano hayo
unapoanza na hata wakifanya majaribio hayo hawapaswi kutumia gari zao
mpya zinazotumika katika msimu husika.
No comments:
Post a Comment