Pages

Friday, June 21, 2013

BAN KI-MOON ALAANI SHERIA YA HABARI YA BURUNDI

Pierre
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameikosoa sheria mpya iliyopitishwa na serikali ya Burundi, ambayo amesema itaathiri uhuru wa vyombo vya habari.
Rais Pierre Nkurunziza, siku ya Jumanne aliridhia sheria hiyo, ambayo imekosolewa vikali na mashirika ya habari na yale ya haki za binaadamu.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky, alisema Katibu Mkuu Ban amesikitishwa na sheria hiyo, yenye vifungu vinavyoweza kukandamiza uhuru wa habari, huku akisisitiza kuwa haki ya uhuru ya kujieleza na sekta huru ya habari ni mambo muhimu kwa ustawi wa demokrasia.
Sheria hiyo iliyopitishwa na bunge la Burundi mwezi April, inadhoofisha ulinzi wa vyanzo vya habari, inadhibiti kuripoti habari za uchunguzi, na inawataka waandishi wote kuwa na shahada ya Chuo Kikuu bila kujali uzoefu.
Pia inapiga marufuku kusambaza taarifa au nyaraka kuhusu mada za ulinzi au taarifa zinazochukuliwa kuwa propaganda za adui, au zinazoweza kuathiri uchumi wa Burundi.
Shirka la kutetea haki za waandishi la Reporters Without Boarders limeielezea sheria hiyo kuwa ni alama ya siku nyeusi kwa uhuru wa habari nchini Burundi.

No comments:

Post a Comment