Rais Jakaya Kikwete
Dar/Dodoma. Rasimu ya Katiba Mpya iliyozinduliwa jana,
imependekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais wa Tanzania maeneo tofauti
ya utendaji wake, ukiwamo uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu wa
Serikali.
Tume hiyo inapendekeza kwamba Rais ashirikiane na
mihimili mingine ya dola katika uteuzi huo, huku ikiwataja Mawaziri na
Naibu Mawaziri, Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi kuwa
uteuzi wao utakapofanywa na Rais lazima uthibitishwe na Bunge.
Mapendekezo hayo ni tofauti na hali ilivyo sasa
wakati uteuzi unaofanywa na Rais hauthibitishwi na Bunge, isipokuwa
nafasi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais itapotokea ikawa wazi kwa sababu
zozote zile.
Pia, tume inapendekeza Rais ashauriane na chombo
kipya kitakachoundwa cha Baraza la Ulinzi la Taifa kuwateua viongozi
wote wa taasisi za ulinzi nchini.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba alisema mfumo wa utawala utaendelea kuwa kama ulivyo hivi
sasa na kwamba, Rais ndiye mtendaji wa Jamhuri ya Muungano na
atachaguliwa moja kwa moja na wananchi.
Jaji Warioba alisema Tume imependekeza mgombea
urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kwamba,
kinga ya kutokuhoji matokeo ya uchaguzi mahakamani iondolewe.
“Mgombea urais anaweza kupendekezwa na chama cha
siasa au kuwa mgombea huru, mgombea wa nafasi hiyo atatangazwa kuwa
mshindi iwapo atakuwa amepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote
zilizopigwa,” alisema Jaji Warioba na kuongeza: “Hata hivyo, matokeo ya
uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa mahakamani, lakini siyo kila mtu
anaweza kufungua kesi, wanaoweza kufungua kesi ni wagombea urais na
Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na mamlaka na uwezo wa kusikiliza
malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe
ndani ya mwezi mmoja, yaani siku 30.”
Alisema Tume inapendekeza Rais achaguliwe moja kwa moja na wananchi na kwamba, suala la umri pia lilijadiliwa kwa upana.
“Wengine walisema umri wa mtu kuruhusiwa kugombea
urais uwe miaka 35 au 50 na kuendelea, Tume imeyachambua maoni yote na
ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za nchi zingine ,” alisema Jaji
Warioba na kuongeza:
“Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo walikuwa na
umri wa miaka 40 au zaidi, kwa kuzingatia maoni ya wananchi, utafiti na
hali halisi, Tume imependekeza Rais aendelee kuchaguliwa na wananchi
pamoja na sifa nyingine mtu atakayegombea Urais asiwe chini ya miaka
40.”
Kutokupunguzwa kwa umri wa urais kutakuwa ni pigo
kwa wansiasa vijana nchini waliopendekeza ushushwe na kuwa miaka 35,
akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Zitto, Makamba watoa kauli.
Akizungumzia suala hilo jana, Zitto alisema uamuzi huo wa umri
hana la kusema, kwa sababu yaliyotolewa ni mapendekezo ya Tume na
kwamba, Chadema watatoa kauli baada ya viongozi kuwasiliana.
Kwa upande wake, Makamba iwapo amebadili msimamo wake, alisema: “Suala la umri siyo kigezo pekee cha kupata uongozi mzuri.”
Makamba alisema ujana wala uzee siyo kigezo cha kumnyima mtu uongozi.
Siku za nyuma Makamba, ambaye ni Mbunge wa
Bumbuli, aliwahi kunukuliwa akitaka umri wa kugombea urais uwe miaka 35
badala ya 40 ya sasa.
Alisema suala la umri lisingemwathiri binafsi, kwani mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 41.
“Ninapongeza Watanzania kwa kutoa maoni yao na kutaka vijana kupewa nafasi za uongozi,” aliongeza Makamba.